Mnamo April  24, 2018  Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Poland, Dr. Abdallah Saleh Possi, alikutana na wadau mbalimbali wa uwekezaji katika mkutano wa kibiashara ulioandaliwa na jumuia ya biashara ya Poland jijini Warsaw. Mkutano huo ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya safari ya kibiashara inayotarajiwa kufanyika mwezi juni mwaka huu. Safari hiyo itahusisha wafanyabiashara kutoka Poland wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania. 

Balozi aliwahimiza wafanyabiashara kutoka Poland kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali, haswa zinazotegemea mali ghafi kutoka nchini, na zenye uwezo wa kutengeneza ajira kwa wananchi wengi, na hivyo kupunguza utegemezi wa uagizaji bidhaa kutoka nje. Sekta hizo ni kama vile madawa, nguo, kilimo na chakula (hussusan uzalishaji wa sukari na mafuta ya kula). Pia balozi aliwahimiza wawekezaji hao kuangalia fursa katima sekta nyingine, haswa nishati mbadala na utalii.

Wahudhuriaji walionyesha kurishishwa na muelekeo wa uchumi wa Tanzania. Licha ya baadhi ya watoa mada kuainisha changamoto mbalimbali, mkutano huu ulitoa taswira ya kujengeka ushawishi miongoni mwa wafanyabiashara wa Poland kuhusiana na uwekezaji Afrika, haswa Tanzania.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa na: Balozi Jerzy Drożdż, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kimataifa kutoka kutoka taasisi ya biashara ya Poland (Polish Chamber of Commerce); Bw. Eugeniusz Rzewuski, Kaimu Balozi wa zamani wa Poland nchini Tanzania; Balozi. Jan Wieliński, Balozi Mstaafu wa Poland katika nchi kadhaa za Afrika; Bw. Robert Zduńczyk, Rais wa Taasisi ya Uchumi Poland-East Africa; Bi, Agata Świtalska-Krych, Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Wielkopolski, mfuko unaosaidia biashara ndogo na za kati, na maendeleo mijini; Bw. Konrad Pawlik, Makamu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland; Bi. Katarzyna Kwiecień, Mkurugenzi wa National Support Center for Agriculture; Bw. Wojciech Rząsiecki, Mkuu wa Idara ya Mikopo ya Serikali (Government Export Credits) Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland; Bw. Łukasz Porażyński, kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Ujasiriamali na Teknolojia ya Poland; Bw. Piotr Maciaszek, mkurugenzi wa Export Credit Insurance Corporation Joint Stock Company (KUKE); Bw. Arkadiusz Zabłoński, Mkurugenzi wa Idara ya Kusaidia Biashara ya Mauzo ya Nje (Department of Export Support, BGK).
 

  • Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Poland, Dr. Abdallah Saleh Possi, akibadilishana mawazo na wadau mbalimbali wa uwekezaji pembeni ya mkutano wa kibiashara ulioandaliwa na jumuia ya biashara ya Poland jijini Warsaw.
  • Wadau mbalimbali wa uwekezaji wa nchi ya Poland wakiwa kwenye mkutano wa kibiashara ulioandaliwa na jumuia ya biashara ya Poland jijini Warsaw uliohudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Poland, Dr. Abdallah Saleh Possi
  • Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Poland, Dr. Abdallah Saleh Possi akiwa na Kiongozi wa Diaspora ya Watanzania nchini Poland Bw. Julius Zellah pamoja na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Poland wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania.
  • Balozi Jerzy Drożdż, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kimataifa kutoka kutoka taasisi ya biashara ya Poland (Polish Chamber of Commerce) akitoa mada kwenye mkutano huo.