MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe ameongoza msafara wa Tanzania kwenda Ujerumani kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya nchi za Afrika Mashariki na Ujerumani.

Ambapo Kongamano hilo limeanza jana  mjini Berlin na washiriki wa Tanzania ni kutoka taasisi za Serikali na wafanyabiashara wa kutoka sekta binafsi.

Imeelezwa kuwa lengo la kushiriki kongamano hilo ni kuvutia wawekezaji wa Ujerumani wenye mitaji, na teknolojia kuja kuwekeza nchini kwenye miradi mbalimbali na pia kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini.

Ujumbe wa Tanzania ulifika Berlin Mei 13, 2018 ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC amoja na timu yake wamefanya kikao pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi. 

Katika mkutano huo Mwambe ameelezea kuwa ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo umejipanga  kwa kunadi fursa za uwekezaji katika sekta za viwanda, afya,  tekinolojia/mawasiliano, nishati na miundombinu.

 Hata hivyo Mwambe ameainisha maeneo mahsusi yanayotafutiwa uwekezaji katika nchi ya Ujerumani kuwa ni ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu na vifaa tiba.

Pia uzalishaji wa umeme mbadala na usambazaji; utekelezaji wa miradi ya miundo mbinu ya usafirishaji ikiwamo reli, viwanja vya ndege , bandari na barabara kwa ujumla na utekelezaji wa mradi wa usalama katika mitandao. 

Kwa upande wa wafanyabiashara imeelezwa kuwa wamejipanga kutafuta wabia katika sekta za ujenzi, utalii, madini, vifaa vya ujenzi na soko la bidhaa mbalimbali za kilimo kama vile , ( mtama, choroko, korosho na mbaazi).

Balozi  Dk.Possi alisisitiza kuwa ni vizuri  mamlaka za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji zipunguze muda wa kuchakata upatikanaji wa vibali hivyo kwani kuchukua  muda mrefu unakatisha tamaa wawekezaji na kuwakimbiza kwenda kuangalia fursa nchi nyingine. 

 Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC amehitimisha mkutano kwa kupongeza juhudi zinazofanywa na Dk. Possi katika kuhamashisha kampuni za Kijerumani pamoja na kuandaa misafara ya wafanyabiashara wa Kijerumani kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.
 
Amefafanuliwa Wajerumani mara zote  hawafanyi bishara ama uwekezaji mahali popote duniani ambapo hakuna uimara wa masuala ya siasa na ukuaji wa uchumi.

Hivyo ujio wa Wajerumani nchini pamoja na nia yao ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ni dhahiri kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania yapo vizuri.

Na yanaendelea kuboreshwa siku hadi siku chini ya serikali ya awamu ya tano  inayoongozwa na Rais Dkt John  Magufuli. 

Mkurugenzi wa TIC  amemhakikishia Balozi Dk.Possi utayari wa TIC kuwapokea wawekezaji kutoka Ujerumani na kuwapatia usaidizi utakaohitajia ili kufanikisha uwekezaji wao nchini. 

Taasisi zinazozoshiriki mkutano huo kutoka Tanznaia ni  TIC, Bohari kuu ya Dawa Tanzania (MSD), Shirika la Umeme Tanzanaia (TANESCO) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).