Tarehe 14 hadi 19 January 2023 Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifanya ziara nchini Uswisi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) uliofanyika tarehe 15 hadi 19 Januari 2024 katika mji wa Davos nchini Uswisi.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais alihudhuria mikutano mbalimbali inayohusu masuala ya uchumi na uwekezaji, utawala bora, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kilimo. Aidha, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifanya mazungumzo ya uwili na viongozi wa mataifa na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani huhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Wakuu wa Taasisi na Makampuni mbalimbali duniani pamoja na Wafanyabiashara.
Kando ya Mkutano huo Mhe. Makamu wa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa Serikali akiwemo Mhe. Demeke Mekonnen Hassen Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ambapo mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Ethiopia katika masuala ya kiuchumi na diplomasia.
Katika hatua nyingine Mhe. Makamu wa Rais alifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Plastic Action Partnership Bi. Clemence Schidm. Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais aliikaribisha taasisi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na taka za plastiki ikiwemo kufanya tafiti zitakazowezesha kutambua aina ya taka za plastiki zinazopatikana kando ya bahari na maeneo ya nchi kavu ili kusaidia kuandaa mkakati wa kukabiliana na changamoto hizo. Pia aliikaribisha Taasisi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kudhibiti taka za plastiki hususani Makao Makuu ya nchi Dodoma.